kwelii hawa hatari sana

YANGA SC imeiadhibu vikali Prisons ya Mbeya kwa kuichapa mabao 5-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.
Ushindi huo unaifanya Yanga SC iendelee kuwa na matumaini ya kutetea taji lake, kwani sasa inatimiza pointi 46 baada ya mechi 21, ikizidiwa pointi nne na Azam FC walio kileleni.
Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Andrew Shamba wa Pwani, aliyesaidiwa na Charles Mbilinyi wa Mwanza na Said Mnonga wa Mtwara, hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0.

Wachezaji wa Yanga SC wakimpongeza Hamisi Kiiza wa pili kushoto aliyefunga mabao mawili leo

Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Arnold Okwi aliifungia Yanga SC bao la kwanza dakika ya 20 kwa shuti la chini la mpira wa adhabu, baada ya yeye mwenyewe kuangushwa nje kidogo ya boksi.
Prisons ilipata nafasi ya kusawazisha bao hilo dakika ya 38, baada beki wa kushoto wa Yanga SC, Oscar Joshua kumsukuma kwenye eneo la hatari Frank Hau, lakini Lugano Mwangama akakosa penalti kwa kupiga juu ya lango la Juma Kaseja.
Mrisho Khalfan Ngassa aliiunganisha nyavuni moja kwa moja vizuri krosi ya Hussein Javu dakika ya 37 kuipatia Yanga SC bao la pili. Kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm alifanya mabadiliko dakika ya 33 kwa kumtoa Jerry Tegete na kumuingiza Hussein Javu.

Mrisho Ngassa wa Yanga SC kushoto akitafuta mbinu za kumtoka beki wa Prisons, Laurian Mpalile kulia

Naipenda Yanga SC; Mrisho Ngassa kushoto akishangilia baada ya kufunga

Kipindi cha pili, Yanga SC walirudi na moto na wao na kufanikiwa kupata mabao matatu zaidi.
Hamisi Kiiza aliyeingia kuchukua nafasi ya Okwi, aliifungia Yanga SC bao la tatu dakika ya 67 akiunganisha krosi ya Simon Msuva.
Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliifungia Yanga SC bao la nne dakika ya 76 kwa penalti, kufuatia Hussein Javu kuangushwa na Nurdin Chona kwenye eneo la hatari.
Diego wa Uganda, Hamisi Kiiza aliifungia Yanga SC bao la tano akimalizia krosi ya Msuva dakika ya 88. Kipindi cha kwanza, Prisons kidogo ilionyesha uhai, lakini kipindi cha pili ilijifia kabisa na Yanga ‘wakamsukuma mlevi’.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Jerry Tegete/Hussein Javu dk33, Mrisho Ngassa/Haruna Niyonzima dk76 na Emmanuel Okwi/Hamisi Kiiza dk59.
Prisons; Beno Kakolanya, Salum Kimenya, Laurian Mpalile, Lugano Mwangama, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Godfrey Mageta/Jimmy Shoji dk68, Freddy Chudu, Peter Michael, Frank Hau na Ibrahim Mamba/Six Mwakasega dk48.

Advertisements

YNGA SPORT CLUB 1 VS AL AHLY

BAO pekee la Nahodha Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ jioni hii limeipa ushindi wa 1-0 Yanga SC katika mchezo wa kwanza wa kuwania kucheza Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Al Ahly ya Misri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Cannavaro alifunga bao hilo dakika ya 87 akimalizia kona maridadi ya winga Simon Msuva kutoka wingi ya kulia.

Kona hiyo ilitokana na kipa Sherif Ekram Ahmed kupangua shuti kali la mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Heileyesus Bazeze aliyesaidiwa na Kindie Mussie Tdedesse Shawangiza  wote kutoka Ethiopia, hadi mapumziko milango ilikuwa migumu.

Shujaa; Beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akipongezwa na wenzake Emmanuel Okwi na SImon Msuva baada ya kufunga bao pekee jioni dhidi ya Al Ahly

Yanga SC ndiyo waliotawala zaidi mchezo na kutengeneza nafasi kadhaa nzuri za kufunga, lakini wakakosa umakini katika kumalizia.

Simon Msuva alikuwa chanzo kizuri cha mashambulizi ya Yanga upande wa kulia, lakini Waganda Emannuel Okwi na Hamisi Kiiza walishindwa kutumia nafasi.

Haruna Niyonzima, Frank Domayo na Mrisho Ngassa kwa pamoja walicheza vizuri katika safu ya kiungo kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili, Ahly kidogo walibadilika na kuongeza kasi ya mashambulizi kupitia kwa Amr Gamal, ambaye hata hivyo alidhibitiwa vikali na walinzi wa Yanga, ambao leo walicheza kwa umakini wa hali ya juu.

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mholanzi Hans van der Pluijm, kumuingiza mshambuliaji Didier Kavumbangu kuchukua nafasi ya Hamisi Kiiza yalifufua makali ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Winga wa Yanga SC, Simon Msuva kushoto akimtoka beki wa Al Ahly
Mshambuliaji wa Yanga SC, Emmanuel Okwi akiwatoka mabeki wa Ahly

Kavumbangu aliwapa wakati mgumu mno mabeki wa Ahly tangu alipoingia dakika ya 66 hata mashabiki wa Yanga wakatamani angekuwa uwanjani tangu mwanzo.

Pamoja na kufungwa 1-0, Al Ahly inayofundishwa na kocha Mohamed Yousef, ilionyesha upinzani kwa Yanga SC, jambo ambalo linaashiria katika mchezo wa marudiano lolote linaweza kutokea.

Baada ya matokeo haya, Yanga SC sasa inahitaji sare ya ugenini ili kusonga mbele hatua ya 16 Bora.

Kihistoria hii inakuwa mara ya kwanza kabisa Yanga SC inapata ushindi dhidi ya timu ya Misri na Kaskazini mwa Afrika kwa ujumla, kwani mara zote imekuwa ikifungwa na kutoa sare.

Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Hamisi Kiiza/Didier Kavumbangu dk66, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa/Said Bahanuzi dk87.

Al Ahly; Sherif Ekramy Ahmed, Saad El-Din Saad, Mohamed Ghareeb, Ahmed El Moneim, Sayed Abdel Waheed, Shihab Eldin Saad, Hossam Mohammed, Ramy Abdel Aziz, Moussa Yedan/Mahmoud Ibrahim dk59, Mohamed Ismail/Ahmed Shakri Abdelraouf dk 73 na Amri Gamal Sayed/Ahmed Raoud Adam dk88.