simba 1 vs azam 2

Simba mpyaAzam-FC3BAO lililofungwa dakika ya 73 na mshambuliaji Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast limeiwezesha Azam FC kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Bara uliochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tcheche alifunga bao hilo akiwa wingi ya kushoto ya uwanja huo na alipiga shuti kali la chinichini akiwa pembeni mwa uwanja (impossible angle) na mpira kutinga wavuni moja kwa moja. Kipa Abel Dhaira wa Simba pengine alidhani mfungaji alipiga mpira huo kama krosi kwenda kwa John Bocco, hivyo hakuwa makini kuzuia mpira huo wa kwanza.

Awali Tchetche alikuwa amepokea pasi kutoka kwa Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ kutoka katikati ya uwanja. Sure Boy alipokea pasi baada ya mshambuliaji wa Simba, Betram Mombeki kupokonywa mpira jirani na katikati ya uwanja.

Ushindi huo wa Azam unaifanya timu hiyo kuishusha Simba kileleni mwa ligi hiyo na kuketi yenyewe ikiongoza kwa pointi 23 ilizopata baada ya kucheza mechi 11 kama ilivyo kwa Simba ambayo inapoteza mechi yake ya kwanza tangu kuanza kwa ligi hii msimu huu.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi 20 ilizopata baada ya kucheza mechi 11, ambapo imeshinda mechi tano na kutoka sare tano. Simba imefunga mabao 21 na kufungwa mabao 10.

Bao la kwanza la Simba lilifungwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ dakika ya 22 akimalizia pasi safi ya Zahor Pazi na kuamsha furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuingia kwa bao hilo, Simba ilionekana kutawala mchezo lakini Azam walizinduka kuanzia dakika ya 35 na kulishambulia lango la Simba kama nyuki na kufanikiwa kupata bao dakika ya 43 mfungaji akiwa ni Tchetche aliyemalizia kazi nzuri ya beki Erasto Nyoni.

Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko matokeo yalikuwa ni bao 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam kufanya mabadiliko ambapo walimtoa beki Said Moradi na nafasi yake kuchukuliwa na David Mwantika ambaye aliweza kupunguza kasi ya mashambulizi ya Simba kwa kiasi fulani.

Dakika 10 baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko baada ya kuwatoa kwa mpigo Zahor Pazi na Amri Kiemba na nafasi zao kuchukuliwa na Sino Augustino na Edward Christopher.

Mabadiliko hayo hayakuweza kuisaidai Simba licha ya mara kadhaa kufika langoni kwa Azam lakini washambuliaji wake Sino Augustino na Mombeki hawakuwa makini kumalizia mipira mingi waliyokuwa wakipewa na viungo.

Tatizo la ukabaji wa nafasi ndilo lililoigharimu Simba na kumfanya Tchetche aifungie Azam bao la pili dakika ya 73.

Katika mchezo wake ujao, Simba itacheza na Kagera Sugar huku Azam ikipambana na Ruvu Shooting.

Advertisements