SIMBA imezidi kujitanua kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara

SIMBA imezidi kujitanua kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Ruvu jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Azam FC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Prisons mjini Mbeya. 
Uwanja wa Taifa, hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Mrundi Amisi Tambwe dakika ya 24 kwa penalti, baada ya beki Jamal Said wa JKT Ruvu kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Hata hivyo, wachezaji wa JKT Ruvu walimzonga mshika kibendera nambari moja, John Kanyenye wa Mbeya aliyetoa penalti hiyo kabla ya kutulia na kuruhusu mkwaju upigwe- na Tambwe akaenda kufunga bao lake la saba katika Ligi Kuu msimu huu ndani ya mechi sita.

Simba mpya

Mabao saba mechi sita; Wachezaji wa Simba SC wakimpongeza Tambwe baada ya kufunga bao la kwanza jioni ya leo

Simba SC ndiyo waliotawala zaidi mchezo kipindi cha kwanza ingawa na JKT Ruvu walikuwa wakishambulia mara kadhaa, lakini ngome ya Wekundu wa Msimbazi ikiongozwa na kipa mrefu zaidi katika Ligi Kuu, Abbel Dhaira ilikuwa imara hii leo.
Simba SC ilipata pigo dakika ya 30, baada ya kiungo wake mahiri, Amri Kiemba kuumia goti na kutoka  nje, nafasi yake ikichukuliwa na Ramadhani Singano ‘Messi’.  
Kipindi cha pili, Simba SC walikianza kwa kasi na kufanikiwa bao la pili dakika nne tu tangu kuanza kwa ngwe hiyo ya lala salama kupitia kwa Ramadhani Singano ‘Messi’.
Messi alifunga bao hilo baada ya kuuwahi mpira uliorudishwa na mabeki wa Ruvu kufuatia Amisi Tambwe kuunganisha krosi maridadi ya Abdulhalim Humud ‘Gaucho’.
Baada ya bao hilo, JKT waliongeza kidogo kasi ya mashambulizi yao, lakini hawakuwa na mipango mwafaka ya kuipenya ngome ya Simba SC.
Mawinga wa JKT walikuwa wakitia krosi za juu langoni mwa Simba wakati washambuliaji wao ni wafupi na kipa wa Wekundu wa Msimbazi, Abbel Dhaira pamoja na mabeki wake, Kaze Gilbet na Joseph Owino ni warefu.
Kwa matokeo hayo, Simba SC inatimiza pointi 14 baada ya kucheza mechi sita na kujiimarisha kileleni mwa ligi hiyo. 

20130421-125940.jpg

Wchezaji wa JKT Ruu wakimzonga refa Anthony Kayombo baada ya kuwapa SImba SC penalti iliyozaa bao la kwanza

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abbel Dhaira, Haruna Shamte, Adeyoum Seif, Kaze Gilbert, Joseph Owino, Abdulhalim Humud, Amri Kiemba/Ramadhani Singano dk29, Said Ndemla, Betram Mombeki/Miraj Madenge dk63, Amisi Tambwe na Haroun Chanongo/Marcel Kaheza dk56. 
JKT Ruvu; Shaaban Dihile, Damas Makwaya, Stanley Nkomola, Omar Mtaki, Jamal Said, Nashon Naftali, Alhaj Zege, Emanuel Swita/Richard Msenya dk58, Bakari Kondo/Paul Ndauka dk78, Salum Machaku na Emanuel Pius.
Katika mechi nyingine, Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Azam FC imetoka sare ya 1-1 na Prisons, bao la Azam likifungwa na Kipre Tchetche dakika ya 49 na la Prisons lilifungwa na Peter Michael dakka ya 36 na Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Ashanti United imetoka sare ya 2-2 na Mtibwa Sugar. Mabao ya Ashanti yalifungwa na Paul Maone na Tumba Swedi, wakati ya Mtibwa yalifungwa na Shaaban Kisiga ‘Malone’.  

Advertisements

MRISHO Khalfan Ngassa leo ameanza kazi vizuri Yanga SC baada ya kuiongoza timu hiyo kupata ushindi wa kwanza ndani ya mechi tano

MRISHO Khalfan Ngassa leo ameanza kazi vizuri Yanga SC baada ya kuiongoza timu hiyo kupata ushindi wa kwanza ndani ya mechi tano, kwa kuilaza Ruvu Shooting ya Pwani 1-0- jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Bao limefungwa na Mganda Hamisi Friday Kiiza, dakika ya 63 akiunganisha kwa tik tak krosi ya Ngassa, ambaye baada ya kupokea pasi ndefu ya Athumani Iddi ‘Chuji’, akamtoka beki wa Ruvu, Stefano Mwasyika.

Amerudi kwa neema; Ngassa ameisaidia Yanga SC kushinda 1-0 Ligi Kuu

Pamoja na ushindi huo, Yanga walikuwa katika wakati mgumu kipindi cha kwanza baada ya kuzidiwa katika eneo la kiungo na Ruvu, iliyoongozwa na Hassan Dilunga katika idara hiyo, akiwafunika Frank Domayo na Haruna Niyonzima.
Lakini kuingia kwa Chuji kipindi cha pili, aliyekwenda kuchukua nafasi ya Domayo, kulileta uhai katika safu ya kiungo ya Yanga na haikuwa ajabu walipofankiwa kupata ushindi.

 

Ngassa na Kiiza wakishangilia

Kwa matokeo hayo, Yanga SC inatimiza pointi tisa baada ya kucheza mechi sita sawa na Azam ambao hata hivyo wamecheza mechi tano, wakati Simba SC waliocheza mechi tano wapo kileleni kwa pointi zao 11.
Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo/Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva/Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbangu, Hamisi Kiiza na Mrisho Ngassa.
Ruvu Shooting; Abdul Seif, Michael Pius, Stefano Mwasyika, George Michael, Shaaban Suzan, Gedion David, Ayoub Kitala/Said Madega, Hassan Dilunga, Cossmas Lewis, Elias Maguri na Reuben Lambele/Kulwa Mfaume.  

AZAM FC imefanikiwa kufuta uteja kwa Yanga SC leo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Azam-FC3AZAM FC imefanikiwa kufuta uteja kwa Yanga SC leo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shujaa wa Azam leo, alikuwa ni kinda aiyepandishwa kutoka kikosi cha pili, Joseph KImwaga ambaye alifunga bao la tatu kwa umahiri mkubwa, baada ya kuuwahi mpira mrefu na kuwazidi mbio mabeki wa Yanga kabla ya kumchambua kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ dakika ya 90.
Lilikuwa bao la kumaliza mchezo na wachezaji wote wa Azam walikwenda kumpongeza Kimwaga nje ya Uwanja upande wa lango la Yanga na waliporejea uwanjani, baada ya dakika moja na ushei filimbi ya kuhitimisha mechi ilipulizwa. 

yanga1
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Dominic Nyamisana, aliyesaidiwa na Charles Simon na Flora Zablon wote wa Dodoma, hadi mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na John Bocco ‘Adebayor’ sekunde ya 34 tu, baada ya kuuwahi mpira uliorudishwa na beki Kevin Yondan kufuatia pigo la kichwa la Brian Umony na kuutumbukiza nyavuni. 
Yanga SC inayofundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts, ilikuja juu baada ya bao hilo na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Azam, lakini hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika hawakufanikiwa kupata bao.
Lakini kipindi cha pili, Yanga walirudi na moto mkali na kufanikiwa kusawazisha bao dakika ya 48 kupitia kwa Mrundi, Didier Kavumbangu aliyeutokea mpira mrefu na kwenda kumchambua kipa wa Azam, Aishi Manula.  
Yanga iliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Azam na kufanikiwa kupata bao la pili, dakika ya 65 mfungaji Hamisi Kiiza aliyemalizia pasi ya Simon Msuva.

Yanga walijiona kama wamemaliza kazi baada ya bao hilo na haikushungaza kibao kilipowageukia na kulala katika mchezo huo.
Beki Kevin Yondan aliunawa mpira kwenye eneo la hatari dakika ya 68 na Kipre Herman Tchetche akaenda kufunga kwa penalti dakika ya 69 na kufanya 2-2.
Yanga wakazinduka na kuongeza mashambulizi langoni mwa Azam kusaka bao la ushindi, lakini shambulizi la kushitukiza la Wana Lamba Lamba liliwamaliza Wana Jangwani dakika ya 90.
Azam waliokoa shambulizi la hatari langoni mwao na kuanzisha shambulizi la haraka- na mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Uhai msimu uliopita, Kimwaga hakufanya makosa- hadi mwisho Azam 3-2 Yanga.
Kwa ujumla mchezo ulikuwa mkali na mashambulizi yalikuwa ya pande zote mbili. Huu unakuwa ushindi wa pili kwa Azam msimu huu ndani ya mechi tano na sasa inafikisha pointi tisa, wakati kwa Yanga SC hiki ni kipigo cha kwanza ndani ya mechi tano, wakiwa pia wametoa sare tatu na kushinda mechi moja, hivyo wanabaki na pointi zao sita.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Jerry Tegete/Hamisi Kiiza dk58 na Haruna Niyonzima.
Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo/Said Mourad dk56, Himid Mao, Farid Mussa/Joseph Kimwaga dk72, Kipre Balou, John Bocco, Humphrey Mieno na Brian Umony/Kipre Tchetche dk52.  
Katika mechi nyingine za ligi hiyo, JKT Ruvu ilifungwa 1-0 na JKT Oljoro Uwanja wa Azam Complex, bao pekee la Paul Malipesa dakika ya 79, Ruvu Shooting ililala 1-0 mbele ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, bao pekee la Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 82.

TIMU zote za wavulana na wasichana zimeingia Robo Fainali katika michuano ya kimataifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars inayofanyika Lagos nchini Nigeria na mshindi atapata Medali, Kombe pamoja na dola za Kimarekani 10,000.
Timu ya wasichana imetinga robo fainali baada ya ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Malawi juzi na kumaliza na  pointi nne katika kundi ambapo timu ya Uganda ikishika uskani kwa point sita. 
Wakicheza kwa kujiami timu ya wasichana ya Tanzania ilipata goli katika dakika ya 17 kupitia kwa mshambuliaji hatari Shelda Boniface, kabla ya Malawi kuzawazisha dakika ya saba katika kipindi cha pili.

Tanzania wavulana

Mshambuliaji mwenye uwezo wa hari ya juu Athanas Mdam alionyesha makeke yake  jana baada ya kufunga magoli matatu (hat-trick) katika mechi dhidi ya Sierra-Leon ambapo Tanzania ilishinda 4-2 na kukata tiketi ya kushiriki hatua inayofata ya michuano ya Mwaka ya kimataifa inayoandaliwa na Airtel.
Mdamu ambaye amedhihirisha kwamba yeye ni liungo muhimu katika michuano hii , alifunga magoli katika dakika ya  6, 48, 56 , Omari Hamisi ndiye aliitimisha goli la nne la Tanzania  katika dakika ya 60. 
Sierra-Leone walipata magoli yao kupitia kwa Mohamed Mustapha katika dakika ya 8 na Alimamy katika dakika ya 14.
Timu ya wavulana ya Tanzania itacheza mechi ya robo fainali na Madagascar leo wakati wasichana watacheza na DRC. Timu ya wavulana itakosa huduma ya mpikaji mabao Athanas Mdamu ambaye yupo majeruhi.
Mshambuliaji hatari Athanas Mdamu ametoa mchango mkubwa sana katika timu mpaka kufikia hatua ya mtoano, amefunga goli kwa kila mechi, dhidi ya Ghana na Zambia. 
“Tutamkosa ila tutapigana mpaka mwisho kuakikisha tuanshinda mechi zote.”Alisema naodha wa timu Thomas Chndeka. Timu nyingine zilizofanikiwa kutinga katika hatua ya robo fainali kwa upande wa wavulana ni mabingwa watetezi Niger, wenyeji Nigeria, Chad, Malawi, Madagascar, Zambia, na Congo. 
Na kwa upande wa wasichana ni mabingwa watetezi Ghana, Nigeria, Chad, Kenya, Uganda, Malawi na DRC.
Mashindano ya kimataifa ya Airtel Rising Stars ni mpango wenye lengo la kuchangia maendeleo ya mpira wa miguu barani Afrika. Pia vijana wanapata fursa ya kuonyesha uwezo na vipaji vyao katika medani ya soka.

SIMBA SC imepunguzwa kasi leo na Mbeya City baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taiafa, Dar es Salaam.

SIMBA SC imepunguzwa kasi leo na Mbeya City baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taiafa, Dar es Salaam. 
Pamoja na matokeo hayo, Simba SC bado inaongoza Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 11 baada ya kucheza mechi tano, wakati Mbeya City inafikisha pointi saba baada ya mechi tano pia. 
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, Charles Mbilinyi na Juma Mwita wa Mwanza, hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-1.

Simba mpya

Simba SC inayofundishwa na mshambuliaji wake wa zamani, Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’, ilipata mabao yake yote kupitia kwa Amisi Tambwe aliyefunga katika dakika za 29 na 33.

Mbeya City, timu ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya inayofundishwa na Juma Mwambusi, bao la la kipindi cha kwanza lilifungwa na Paul Nonga dakika ya 37, wakati la kusawazisha lilifungwa na Richard Peter dakika ya 69.
Tambwe alifunga bao lake la kwanza akiunganisha krosi ya Chanongo, wakati la pili ilikuwa pasi ya Betram Mombeki.
Paul Nonga alifunga bao lake kwa shuti kali ambalo lilimshinda kpa wa Simba SC, Abbel Dhaira Peter alifunga bao lake akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Mwagane Peter.

3eb07-20

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abbel Dhaira, William Lucian ‘Gallas’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Kaze Gilbert/Hassan Hatibu dk66, Joseph Owino, Jonas Mkude, Twaha Ibrahim/Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dk50, Amri Kiemba/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk79, Betram Mombeki, Amisi Tambwe na Haroun Chanongo. 

Mbeya City; David Burhan, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Deogratius Julius, Antony Matogolo, Yohana Morris, Mwagane Yeya/Richard Peter dk59, Steven Mazanda, Paul Nonga, Deus Kaseke na Yussuf Willson.   
Katika mechi nyingine, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wenyeji Mgambo Shooting Stars walitoka sare ya 1-1 na Rhino Rangers ya Tabora, Prisons ilitoka 1-1 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya, wakati Kagera Sugar ilishinda 3-0 dhidi ya Ashanti United ya Dar es Salaam Uwanja wa Kaitaba.
Ligi hiyo itakamilisha mzunguko wake wa tano kesho kwa mechi tatu moja ndiyo hiyo ya Azam na Yanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku JKT Ruvu ikikwaruzana na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Ruvu Shooting inayokamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi itakuwa mgeni wa Coastal Union katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.