Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameita kambini wachezaji 24 kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameita kambini wachezaji 24 kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia 6246f-5s

Wachezaji hao wanatakiwa kuripoti kambini Agosti 29 mwaka huu kabla ya saa 1 kamili usiku. Kambi ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa kwenye hoteli ya Accommondia jijini Dar es Salaam.

 

Makipa walioitwa katika timu hiyo Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Nadir Haroub (Yanga), Erasto Nyoni (Azam), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar) na David Luhende (Yanga).

 

Viungo Khamis Mcha (Azam), Salum Abubakar (Azam), Said Dilunga (Ruvu Shooting), Frank Domayo (Yanga), Athuman Idd (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Amir Kiemba (Simba), Mrisho Ngasa (Yanga), Simon Msuva (Yanga), John Boko (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) na Juma Liuzio (Mtibwa Sugar).

 

RAMBIRAMBI MSIBA WA BARAKA KITENGE

Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Yanga na Taifa Stars, Baraka Kitenge (74) kilichotokea leo mchana (Agosti 20 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

 

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Kitenge akiwa mchezaji, alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

 

Kitenge amefia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo alikuwa amelazwa akisumbuliwa na kansa ya uti wa mgongo. Enzi zake katika Yanga na Taifa Stas alicheza na wachezaji kama akina Athuman Kilambo na Abdulrahman Juma.

 

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kitenge, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Yanga na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

 

Mipango ya mazishi inafanywa nyumbani kwa Marehemu, Yombo Vituka (Jet) jijini Dar es Salaam. Mungu aiweke roho ya marehemu Kitenge mahali pema peponi. Amina

Advertisements

poleni fan wa AZAM FC

AZAM FC1AZAM FC leo imehitimisha ziara yake ya Afrika Kusini kwa kipigo cha bao 1-0 mbele ya wenyeji, Moroka Swallows kwenye Uwanja wa Volkswagen Dobsonville mjini Soweto.
Huo unakuwa mchezo wa tatu kwa washindi hao wa pili wa Ligi Kuu Bara misimu miwili mfululizo kufungwa hapa, baada ya awali kuchapwa 3-0 na Kaizer Chiefs, 2-1 na Orlando Pirates, wakati mchezo pekee iliyoshinda ni dhidi ya Mamelodi Sundowns 1-0.
Katika mchezo wa leo, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika bila bao, huku wageni ndiyo wakipoteza nafasi tatu za kufunga, mbili kupitia kwa Khamis Mcha ‘Vialli’ na moja Himid Mao.

Ilikuwa dakika ya 40, wakati Mcha alipopewa pasi nzuri na Jabir Aziz, lakini akiwa amebaki na kipa akagongesha mwamba na mpira ukarudi uwanjani, ukamkuta Himid Mao kwenye nafasi nzuri, akapiga juu ya lango.
Awali ya hapo, Mcha tena alipewa pasi nzuri na Waziri Salum, lakini akiwa amebaki na kipa akapiga shuti lililomlenga kipa, akadaka dakika ya 37.
Kipindi cha pili, Moroka walibadilisha karibu timu nzima na miongoni mwa walioingia ni mshambuliaji mkongwe wa kimataifa wa Afrika Kusini, SIyabonga Nomvette.
Nomvette ambaye pamoja na kuonekana kasi yake imepungua, ameonyesha bado ana uwezo na alipata nafasi nzuri ya kufunga akiwa amebaki na kipa dakika ya 75, lakini shuti lake likapanguliwa na kipa Aishi Manula na kuwa kona, ambayo haikuzaa matunda.
Moroka ilipata bao lake pekee dakika ya 70, mfungaji Mnigeria, Felix Obada aliyetokea pembeni na kufumua shuti akiwa nje ya 18.
Azam ambayo nayo pia ilibadilisha karibu timu nzima iliyoanza, ilijitahidi kusaka bao la kusawazisha, lakini bahati haikuwa yao.
Kocha Mreno wa Moroka, Zeka Marquees aliisifu Azam baada ya mechi hiyo kwamba ni timu nzuri na akaitabiria kufika mbali katika Kombe la Shirikisho mwakani.
Muingereza Stewalt Hall wa Azam alisema timu yake ilicheza vizuri na ilishindwa kutumia nafasi ilizopata, wakati wapinzani walitumia nafasi yao.
Baada ya mchezo wa leo, Azam inatarajiwa kuondoka kesho asubuhi kwa ndege ya Afrika Kusini kurejea nyumbani, Dar es Salaam na Agosti 17, itacheza mechi ya kuwania Ngao, dhidi ya Yanga SC Uwanja wa Taifa.
Kikosi cha Azam FC leo kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni/Joackins Atudo dk46, Waziri Salum/Samih Hajji Nuhu dk46, Said Mourad/David Mwantika dk46, Aggrey Morris, Jabir Aziz/Kipre Balou dk46, Kipre Tchetche, Himid Mao, Gaudence Mwaikimba/John Bocco dk46, Ibrahim Mwaipopo/Mudathir Yahya dk80 na Khamis Mcha/Seif Abdallah dk80.

MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga SC, Hussein Javu leo amefunga bao lake

MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga SC, Hussein Javu leo amefunga bao lake la pili tangu ajiunge na klabu hiyo majira haya ya joto, akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro baada ya kuiwezesha timu yake hiyo mpya kushinda 1-0 dhidi ya 3Pillars ya Nigeria, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hilo linakuwa bao la pili kwa Javu tangu atue Yanga akifunga katika mechi mbili mfululizo, baada ya mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar kufunga bao moja akitokea benchi kipindi cha pili, Yanga ikishinda 3-1, mabao mengine yakifungwa na Jerry Tegete na Said Bahanuzi, wakati la timu yake ya zamani lilifungwa na Shaaban Kisiga ‘Malone’.
                 
                                                      Mshambuliaji wa Yanga Hussein Javu akiitoka ngome ya 3 Pillars.
                 
                                                                                                     Mrisho Ngassa kazini.

Katika mchezo wa leo, mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara Young Africans waliingia uwanjani kwa lengo la kusaka ushindi na kuendeleza rekodi ya ushindi katika michezo ya kirafiki ya kujipima nguvu inayocheza kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom 2013/2014.
Ikiwa tumia washambuliaji wake wapya Hussein Javu na Mrisho Ngassa waliojiunga na kikosi msimu huu, Yanga ilikosa nafasi za wazi za kufungua kupitia kwa washambuliaji hao ambao hawakuonekana kuwa makini makini katika umaliziaji wa mipira iliyokuwa ikiwafikia.
David Luhende alikosa bao dakika ya 34 kufuatia mpira alioupiga kuokelewa na mlinda mlango wa 3Pillars FC na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda, huku awali Said Bahanuzi akikosa nafasi pia kama hiyo dakika ya 17 ya mchezo.
Hussein Javu aliipatia Young Africans bao kwanza dakika ya 40 ya mchezo kwa ustadi akiitumia vizuri nafasi hiyo aliyopewa na kuingo Athuman Idd ‘Chuji’ aliyewazidi ujanja walinzi wa 3Pillars FC na kumpasia Javu aliyeukwamisha mpira wavuni na kuhesabu bao kwa watoto wa Jangwani.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Young Africans  -0  3Pillars FC.

           
                                                                                         Benchi la Yanga SC.
           
                                                   Jerry Tegete akiipangua safu ya ulinzi ya 3 Pillars.
          
                                                                                                        Kikosi cha Yanga.
          
                                                                                         Kikosi cha 3 Pillars.
         
Timu zikiingia uwanjani. (PICHA NA RICHARD BUKOS/GPL)Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko ambapo Yanga iliwaingiza Didier Kavumbagu, Kelvin Yondani, Oscar Joshua, na Salum Telela kuchukua nafasi za Nadir Haroub, Jerson Tegete, Juma Abdul na Said Bahanuzi mabadiliko ambayo yaliongeza kasi ya mchezo.
David Luhende ambaye leo alikuwa mwiba kwa timu ya 3Pillars FC nusura aipatie Yanga bao la pili lakini mpira alioupiga ulikokolewa na walinzi wa timu hiyo ya Nigeria na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Yanga iliendelea kulishambulia lango la 3Pillars dakika zote za mchezo lakini kutokua makini kwa mshambuliaji Didier Kavumbagu na Hussein Javu kuliendelea kuufanya ubao wa mabao uendelee kusomeka 1-0.
Mpaka dakika 90 za mwamuzi Oden Mbaga zinamalizika, Young Africans 1-0 3Pillars FC .
Kesho kikosi cha Yanga hakitakua na mazoezi na wachezaji wote watakua na mapumziko kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Eid na waterejea tena mazoezini siku ya jumamosi asubuhi katika uwanja wa Loyola kuendelea kujifua na maandalizi ya Ligi Kuu.
Young Africans: 1.Ally Mustapha ‘Barthez’, 2.Juma Abdul/Salum Telela, 3.David Luhende, 4.Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Kelvin Yondani, 5.Rajab Zahir, 6.Athuman Idd ‘Chuji/Issa Ngao, 7.Said Bahanuzi/Abdallah Mguhi ‘Messi’/Shaban Kondo, 8.Haruna Niyonzima/Bakari Masoud, 9.Jerson Tegete/Didier kavumbagu, 10.Hussein Javu, 11.Mrisho Ngassa

BAO pekee la Gaudence Exavery Mwaikimba jioni ya leo

4c77a-azam252bvitBAO pekee la Gaudence Exavery Mwaikimba jioni ya leo, limeipa ushindi wa 1-0 Azam FC ya Dar es Salaam katika mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji Mamelodi Sundwons kwenye Uwanja wa mazoezi wa timu hiyo, uliopo Chloorkop, Johannesrbug mjini hapa.
Huo ulikuwa mchezo wa pili kwa Azam FC katika ziara yao ya nchini hapa kujiandaa na msimu baada ya juzi kufungwa mabao 3-0 na Kaizer Chiefs.
Katika mchezo wa leo, hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na wenyeji ndiyo waliotawala zaidi mchezo kipindi hicho, ingawa Azam walifanikiwa kutengeneza nafasi nzuri zaidi ya kufunga.

Khamis Mcha ‘Vialli’ aliingia vizuri ndani kutokea pembeni kushoto hadi ndani ya eneo la hatari na akampa pasi ya ‘hapa kwa hapa’ John Bocco ‘Adebayor’ akiwa anatazamana na lango, lakini akapiga juu ya lango dakika ya 43.
Kipindi cha pili Azam waliingia kwa ari mpya na kufanikiwa kuuteka mchezo hali ambayo ilisababisha wafanye mashambulizi mengi langoni mwa Mamemlodi.
Almanusra Bocco afunge dakika ya 65 kama si kichwa chake kupaa juu ya lango kufuatia krosi maridadi ya Kipre Herman Tchetche.
Mamelodi walijibu shambulizi hilo dakika ya 70 na shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 19 lililopigwa na Jabu Shongwe liligonga nguzo ya juu ya lango na kurejea uwanjani kabla ya Said Morad ‘Mweda’ kuondosha kwenye hatari.
Katika dakika ya 74, Mwaikimba aliyeingia uwanjani dakika ya 64 kumpokea Bocco aliunganisha vizuri kwa kichwa krosi ya beki Joackins Atudo kutoka wingi ya kulia, ambaye pia alitokea benchi kipindi cha pili kuipatia Azam bao pekee kwenye mchezo wa leo.
Dakika ya 89 Mwaikimba alikaribia tena kufunga kama si shuti lake kupaa juu ya lango akiwa ndani ya eneo la hatari kufuatia krosi nzuri ya Tchetche.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall alifurahia matokeo na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake na pia akasifu ushindani ulioonyeshwa na wapinzani.
Kwa wake, Pitso Masomane kocha wa Mamelodi alisifu Azam na akasema kwa soka waliyoonyesha hastaajabu kwa nini wameshika nafasi ya pili katika Ligi Kuu. Katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni/Joackins Atudo dk 46, Waziri Salum/Samih Hajji Nuhu dk 80, Said Morad/David Mwantika dk77, Aggrey Morris, Jabir Azzi/Kipre Balou dk50, Himid Mao/Ibrahim Mwaipopo dk55, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Mudathir Yahya dk75, John Bocco/Gaudence Mwaikimbadk65, Kipre Tchetche na Khamis Mcha/Seif Abdallah dk85.
Sundown; Wayne Shandialands/Glenn dk78, Ramahlwe Mphanhlele, Punch Masenamela, Rashid Sumaila, Emanuel Mathias, Thami Sangweni/Sibusiso Khumalo dk51, Jabu Shongwe/Raymond Monama dk62, Mzikayise Mashaba, Richard Hanyekane, Elias Pelembe dk73, Surprise Moriri/Mphela Katlego dk79 na Katlego Mashego.

musa hasan mgosi hivi karibuni atajiunga na mtibwa sugar

MGOSI1mussa mgosiMshambuliaji wa zamani wa klabu ya Simba Mussa Hassan Mgosi amejiunga rasmi na klabu ya Mtibwa Sugar ya Manungu Morogoro.

Mgosi ambaye msimu uliopita alikuwa akiitumikia klabu ya JKT Ruvu amejiunga na Mtibwa kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Akiongea na mtandao huu, kocha wa Mtibwa Sugar  Mecky Mexime amethibitisha kwamba klabu yake imemsajili mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba, “Mgosi anakidhi vigezo vya mshambuliaji tunayemhitaji baada ya kuondoka wa Javu aliyejiunga na Yanga. Ameshaini mkataba wa mwaka mmoja na atajiunga na kambi ya maandalizi ya msimu mpya hivi karibuni.”

AZAM FC LEO WATEMBEZEWA KICHAPO

AZAM FC imeanza vibaya ziara yake ya mechi za kujipima nguvu mjini hapa, baada ya kufungwa mabao 3-0 na wenyeji, Kaizer Chiefs katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa mazoezi wa wa timu hiyo, eneo la Nachurena.
Azam iliyoondoka nchini jana mchana kwa ndege ya Shirika la Afrika Kusini, kuja Johannesburg, Afrika Kusini kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na msimu mpya, katika mchezo wa leo iliathiriwa na uchofu wa safari na hali ya hewa ya baridi, hivyo kucheza chini ya kiwango.

FZAKAR
                                                                     AZAM FC

Timu hiyo yenye maskani yake, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, iliyoondoka na kikosi chake kizima, kasoro wachezaji wawili tu majeruhi, kiungo Mkenya, Humphrey Mieno na mshambuliaji Mganda, Brian Umony, imefikia katika hoteli ya Randburg Towers.
Azam jana ilifanya mazoezi yake ya kwanza kwenye Uwanja wa Wits University asubuhi na jioni na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Muingereza Stewart Hall amefurahishwa na mazingira ya kambi na Uwanja wa mazoezi.
Baada ya mchezo wa leo, Azam itashuka tena dimbani Agosti 7, kumenyana na Mamelodi Sundowns kabla ya kuivaa Orlando Pirates Agosti 9 na Agosti 12 itamaliza ziara yake kwa kumenyana na Moroka Swallows.
Azam inatarajiwa kurejea nchini Agosti 13 tayari kwa mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii kuashiria kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Yanga SC, Agosti 17, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Safari hii Azam, washindi wa pili mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu wamepania kutwaa Ngao mbele ya Yanga, baada ya mwaka jana kufungwa na Simba SC na kocha Muingereza Stewart Hall anajiandaa kikamilifu kwa ajili hiyo.