AZAM imerejea katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kishindo leo baada ya kutoa kipigo kikali cha magoli 4-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika mechi ya kwanza chini ya kocha mpya, Stewart Hall, aliyerejea kuifundisha timu hiyo kwa mara ya pili.

Hall, ambaye alifukuzwa katika timu hiyo baada ya kutofautiana na uongozi kabla ya kutua katika klabu ya Sofapaka ya Kenya aliyokuwanayo hadi aliporejea nchini jana usiku, aliendeleza rekodi yake nzuri na Azam akiisaidia kurejea katika nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 21, mbili nyuma ya vinara Simba na Yanga wenye pointi 23 kila moja. Azam bado ina mechi moja mkononi. Coastal imeshuka hatua moja hadi nafasi ya nne ikiwa na pointi 19. 


Kagera Sugar ilijiimarisha katika nafasi yake ya tano kwa kufikisha pointi 17 baada ya kuifunga Toto African 2-1 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza katika mechi nyingine pekee ya ligi kuu iliyochezwa leo.


Kwenye Uwanja wa Azam Complex, Gaudence Mwaikimba, ambaye amekuwa akikaa benchi kwa muda mrefu katika mechi za chini ya kocha aliyetimuliwa Mserbia Boris Bunjak, alilipa fadhila za kuaminiwa na Hall kwa kufunga goli la kuongoza la Azam katika dakika ya 23 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Khamis Mcha.


Kipre Tchetche alifunga goli lake la sita la msimu na kuungana na Didier Kavumbagu wa Yanga kuongoza chati ya wafungaji, baada ya kumpiga chenga kipa wa Coastal, Jackson Chove aliyeachwa akiwa ameanguka chini katika dakika ya 36.


Mcha, aliyekuwa nyota wa mchezo, aliifungia Azam goli la tatu baada ya kupokea pasi fupi ya Said Morad na kupiga shuti la kustukiza lililomshinda Chove aliyeruka bila ya mafanikio na kushuhudia timu hizo zikienda mapumziko huku wenyeji wakiwa mbele kwa magoli 3-0.


Jioni nzuri ya Mcha ilikamilika pale alipoifungia Azam goli la nne katika dakika ya 73 kwa kupiga shuti lililomgonga Othman Tamim wa Coastal na kutinga wavuni na wachezaji wa Azam walithibitisha wanavyompenda kocha wao aliyerejea Hall kwa kushangilia bao hilo kwa kumfuata mahala alipo na kumpigia makofi.


Kiungo Mkenya Jerry Santo aliifungia Coastal, ambayo haikuonyesha upinzani uliotarajiwa, goli la kufutia machozi dakika tatu kabla ya mechi kumalizika akitumia pasi ya fupi ya Salim Gilla. 


Baada ya mechi hiyo, kocha Hall alisema amefurahishwa na ushindi na kwamba siri ya ushindi iko mikononi mwa wachezaji ambao wamethibitisha kwamba walikuwa wakimhitaji arejee.


Kuhusu sababu za kurejea nchini, Hall alisema njaa ilimkimbiza Sofapaka ambako alidai kwamba wachezaji hawajalipwa kwa miezi minne sasa na kwa kuwa Azam anaipenda moyoni mwake, alipopata tu ofa ya kurejea alikubali mara moja. 


Azam itaikabili Yanga Jumapili katika mechi yao ijayo ya Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Taifa wakati vinara Simba watakuwa ugenini Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri Jumamosi.


Vikosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi vilikuwa; 

Azam: 
Ally Mwadini, Kipre Tchetche, Salim Nuhu, Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris, Said Mourad, Kipre Bolou/ Ibrahim Mwaipopo (dk.69), Jabir Aziz Stima, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/ Himid Mao (dk.76), Gaudence Mwaikimba/ Abdi Kassim ‘Babi’ (dk.80), Kipre Tchetche na Mcha Khamis.

Coastal Union:

Jackson Chove, Said Sued, Juma Jabu, Mbwana Hamis, Jamal Machelenga/ Salim Gilla (dk.41), Jerry Santo, Seleman Kassim ‘Selembe’, Razaq Khalfani/ Khamis Shango (dk.77), Daniel Lianga, Green Atupele/ Dayton Lameck (dk.63), Othman Tamim.    

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s